Vijana kuwezeshwa kupitia ardhi

0
147

Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali imetenga hadi ekari 10 kwa kila kijana mwenye sifa, ambapo baadaye watazimiliki. 

Rais Samia amesema Tanzania iko katika mchakato wa kupokea maombi kwa kundi la kwanza la vijana watakaopata fursa ya kupata mafunzo ya miezi mitatu kuanzia mwezi Februari mwaka huu, ili baadaye wagaiwe ardhi.  

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo huko Dakar, Senegal alipokuwa akijibu swali kuhusu mikakati ya serikali katika kuvutia vijana kushiriki kwenye kilimo, upatikanaji wa ardhi, teknolojia na fedha , wakati wa ufunguzi wa mkutano unaohusu kilimo.

Amesema benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itatoa mkopo wa dola milioni 120 za Kimarekani kwa Tanzania kwa ajili ya sekta ya kilimo ikiwemo umwagiliaji na kujenga kituo cha usafirishaji na usambazaji mbolea.

Mpango huo unaowalenga vijana na wanawake unajulikana kama BBT, ‘Ujenzi wa Kesho Bora’  ambapo pia umeanzisha mfuko wa dhamana kwa vijana na huduma za mikopo nafuu chini ya Mfuko wa Pembejeo.  

Rais Samia amesema Tanzania imeamua kuanzisha mpango huo kutokana na idadi kubwa ya vijana kukosa sifa zinazohitajika na taasisi za fedha wanapoomba mikopo na kwamba tangu kuanzishwa kwa mpango huo miezi sita iliyopita, tayari ekari laki sita zimetengwa nchi nzima na kazi ya kusafisha maeneo hayo imeanza.