Mshambuliaji wa Mancherster City, Erling Haaland anaendelea kuifanya Ligi Kuu ya England namana anavyotaka yeye kutokana na namna anavyovunja na kuweka rekodi kadiri ligi inavyoendelea.
City ikiwa imeshuka dimbani mara 20 katika ligi, tayari Haaland amefunga magoli 25, akiwapita wafungaji bora wa ligi hiyo kwa misimu mitatu iliyopita ambao walikuwa na magoli 23 katika michezo 38.
Akiendelea kuzifumania nyavu, Alan Shearer ndiye mchezaji pekee mwenye rekodi ya kuwa na hattrick nyingi (5) kwa msimu mmoja wa EPL kumzidi Haaland ambaye hadi sasa amefikisha hattrick nne, huku akiamini huenda ataivunja rekodi hiyo.
Aidha, raia huyo wa Norway amefunga magoli 18 katika michezo 11 ambayo City imecheza nyumbani, akiwa ndiye mchezaji wa klabu hiyo mwenye magoli mengi katika msimu mmoja akimpita Sergio Aguero aliyefunga magoli 16 msimu wa 2011/12.
Akiwa bado ana michezo 18 ya ligi, mengi yanatarajiwa kutoka kwake ikiwa ni pamoja na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa.