Mbowe ammwagia sifa Rais Samia Mkutano wa CHADEMA

0
258

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kuridhia maridhiano ambayo yanalenga kuwaunganisha Watanzania .

Akizungumza katika mkutano wa ufunguzi wa mikutano ya hadhara ya chama hicho, Mbowe amesema kuwa amefanya vikao vingi na Rais Samia, na kwamba kwa pamoja waliamua kuweka pembeni masilahi ya vyama vyao ili waweze kujenga Taifa lenye umoja.

“Sitaacha kutambua ustahimilivu wa Rais Samia Suluhu Hassan na ustahimilivu wa Abdulrahman Kinana. Hawa ni watu wawili ambao nilisimama nao kupigana kuitafuta Tanzania bora ya kesho,” amesema.

Aidha, ametumia mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza kuwakosoa viongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho ambao wanaeneza kile alichokiita kuwa ni propaganda kwamba “Mbowe amelamba asali,” ili kuiacha misingi wa chama hicho cha upinzani.

“Yeyote mwenye ushahidi, anayeua reputation [heshima] na uaminifu wangu kwamba Mbowe nimekula senti tano, asimame aseme. Mambo ya kuumizana, kudhalilishana, siwezi nikayakubali,” amesema huku asisitiza kuwa amepoteza mabilioni ya fedha katika harakati za kupigania haki.

Hata hivyo, amesema yuko tayari kuwasamehe wote waliozusha maneno hayo, na waanze upya katika safari ya kukijenga chama hicho na kupigania katiba mpya na tume huru ya uchaguzi kueleka uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, na uchaguzi mkuu mwaka 2025.

Mkutano huo umefanyika ikiwa ni takribani wiki tatu tangu Rais Samia alipotangaza kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, huku akihimiza wanasiasa kufanya siasa za kistaarabu, zisizohusisha matusi na vurugu.