Kisanduku cha ndege ya Ethiopia kupelekwa nje

0
430

Serikali ya Ethiopia imesema kuwa itakipeleka kisanduku cha kurekodia mwenendo wa ndege yake aina ya Boeing 737 MAX 8, iliyoanguka nchini humo Jumapili iliyopita nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Ethiopia imetoa tangazo hilo huku tayari nchi kadhaa zikiwa zimesimamisha usafirishaji wa abiria kwa kutumia ndege hizo zinazotengenzwa nchini Marekani, baada ya ndege hiyo kuanguka na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwa ndani yake.

Hata hivyo Marekani imeendelea kusisitiza kuwa ndege zake hizo aina ya Boeing 737 MAX 8 ni salama kwa usafiri wa anga, licha ya ajali ya hiyo ya Ethiopia kutokea ikiwa imepita miezi mitano tu tangu ajali nyingine kama hiyo kutokea.

Ndege nyingine kama hiyo ilianguka nchini Indonesia, muda mfupi mara baada ya kuruka na kusababisha vifo vya abiria wote 180 waliokuwa ndani yake, hali ambayo imesababisha hofu miongoni mwa wasafiri.

Miongoni mwa mataifa yaliyositisha usafiri wa ndege hizo ni China ambayo imenunua ndege Mia Moja  kutoka Marekani pamoja na Nigeria.

Serikali ya Ethiopia kwa mara ya kwanza imewaruhusu ndugu za watu waliokuwa katika ajali hiyo ya ndege kwenda mahali ambapo ndege hiyo ilianguka ili kushuhudia kile kilichotokea.