Miradi ya dola bilioni 3.68 yasajilIwa TIC

0
705

Waziri Mlkuu Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, miradi mipya ya uwekezaji 630 yenye thamani ya dola bilioni 3.68 za kimarekani inayotekelezwa na kampuni za India imesajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Amesema hatua hiyo inatokana na jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya uwekezaji zinazofanywa na Serikali.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka India kuwekeza Tanzania.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa bunge la India ulioongozwa na Spika wa Bunge hilo OM Birla.

Amesema India na Tanzania zimekuwa na ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na biashara, huku India ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na ushirikiano wa biashara unaofikia dola bilioni 4.58 za Kimarekani kwa mwaka 2021/ 2022.

“Rais ana matumaini makubwa na ushirikiano uliopo baina ya nchi ya Tanzania na India na kwamba ushirikiano huo umekuwa na manufaa makubwa kati ya nchi zetu”. amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Kwa upande wake Spika wa Bunge la India Birla amesema, bunge la India litakuwa msemaji mzuri wa ushirikiano na maendeleo baina ya Tanzania na nchi hiyo ili nchi hizo ziendelee kunufaika na ushirikiano uliopo.