Uchumi wa Tanzania wazidi kupaa

0
128

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema anategemea uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 5 kwa mwaka 2023 kulinganisha na mwaka 2022 ulipokua kwa asilimia 4.7 na mwaka 2021 asilimia 4.3

Akizungumza na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa katika sherehe ya mwaka mpya 2023 ya chakula cha jioni (Diplomatic Sherry Party) amesema ni matarajio yake kuwa uchumi utazidi kukua kutokana na usimamizi mzuri wa uchumi ambapo Tanzania imetajwa na Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Afrika katika eneo hilo.

Amesema usimamizi huo unatokana na mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kubadilisha mazingira ya kibiashara yaliyohamasisha sekta binafsi kurejesha masoko hivyo kupelekea kuongezeka kwa uwekezaji wa moja kwa moja nchini.

Aidha, kwa upande mwingine amesema kumekuwa na ongezeko la miradi nchini ambapo kwa mwezi Julai hadi Novemba 2022 kumeshuhudiwa kuongezeko kwa miradi iliyofikia 132 yenye thamani ya dola bilioni 3.16 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na idadi ya miradi iliyosajiliwa kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2021.

Rais Samia amefanya mazunguzo na mabalozi hao na kufanya sherehe hiyo ya mwaka mpya 2023 katika Ukumbi wa Kikwete, Ikulu jijini Dar es Salaam.