Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu amesema kuwa atarejea nchini Januari 25, 2023, akitokea nchini Ubelgiji, ili kushirikiana na viongozi wengine wa chama hicho katika shughuli za kisiasa nchini.
“Ninapenda kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa, nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya tarehe 25 Januari, 2023, majira ya saa saba na dakika 35 mchana,” amesema Lissu akizungumza kwa njia ya mtandao.
Aidha, ametumia jukwaa hilo kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha nia ya kuleta mageuzi ya kisiasa nchini, ikiwemo kukwamua mchakato wa katiba akisema kuwa “tunawajibika kumjibu Mheshimiwa Rais kwa kuonyesha, na kudhihirisha kwa vitendo, kwamba na sisi pia tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo.”
“Ninarudi nyumbani kuja kushiriki katika kuandika ukurasa wa kwanza mpya wa kitabu chenye kurasa 365 cha mwaka huu wa 2023. Ninaamini kwamba, kwa umoja wetu na kwa mapenzi yetu kwa nchi yetu, tutaandika kitabu kizuri,” ameongeza Lissu ambaye alikuwa mgombea Urais kupitia CHADEMA mwaka 2020.