Redio za TBC kusikika nchi nzima mwaka 2024

0
324

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema hadi kufikia mwaka 2024 usikivu wa matangazo ya TBC Taifa na TBC FM utakuwa nchi nzima.

Dkt. Rioba amesema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kituo cha kurusha matangazo ya redio kilichopo Inyonga, Mlele mkoani Katavi.

Aidha, Dkt. Rioba amesema kutokana na mabadiliko ya teknolojia, mitambo ya zamani ya redio haifanyi kazi kwa sababu ya ukosefu wa vipuri baada ya viwanda kufungwa na kuhitaji uwekezaji mpya ambao ni ujenzi mpya wa vituo hivyo ambao unafanywa hivi sasa.

“TBC imekamilisha miradi mingine ya upanuzi katika vituo 7 ambavyo ni; Karagwe-Kagera, Bunda-Mara, Kahama-Shinyanga, Sikonge-Tabora, Kisulu-Kigoma, Nkasi-Rukwa na Same-Kilimanjaro,” amesema Dkt. Rioba.

Hata hivyo Dkt. Rioba amesema katika mwaka wa fedha 2022/23, TBC imeanza utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa usikivu katika vituo 9.

Pia katika mwaka wa fedha 2022/23, Dkt. Rioba amesema TBC kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imeanza utekelezaji wa miradi ya upanuzi wa usikivu katika vituo 5 ambavyo ni Chunya-Mbeya, Kiteko-Manyara, Chemba-Dodoma, Kyerwa-Kagera na Mkinga-Tanga ambapo miradi hii imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.9.

“TBC imejizatiti kuhakikisha usikivu unawafikia wananchi wote kwa kuwekeza miundombinu ya utangazaji na jukumu hili la kupeleka usikivu kwa wananchi maeneo yote ya nchi,” amesema Dkt. Rioba

InyongaMlele #Katavi #TBCredio #TBCtaifa #TBCfm #TBCupdates #TBConline