Zaidi ya wanafunzi milioni 1 wanatarajiwa kuanza masomo yao ya kidato cha kwanza nchi nzima leo, Serikali ikiendelea kusisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi ya shule kwa uhaba wa madarasa.
Kwa mwaka wa pili sasa, Serikali imeweza kuhakikisha wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza wanaanza kwa pamoja baada ya kujenga madarasa ya kutosha na kuondoa utaratibu wa kipindi cha nyuma ambapo wanafunzi walichelewa kuanza shule wakisubiri machaguo ya pili, tatu au zaidi.
Katika muhula unaoanza leo Januari 9, 2023, wanafunzi 1,073,941 wamechaguliwa ambapo kati yao wavulana ni 514846 na wasichana ni 559,095.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Rais Samia Suluhu Hassan aliandika “… hakuna mwanafunzi atayekosa nafasi ya shule kwa uhaba wa madarasa,” ambapo kwa miaka miwili amewezesha ujenzi wa madarasa 23,000.
Kwa mujibu wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano unaotekelezwa kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26, Serikali ilipanga kujenga vyumba vya madarasa 4,040 kwa ajili ya shule za sekondari, lakini kwa mwaka 2022 pekee imejenga madarasa 8,000 ambayo yanaanza kutumika leo.