Jonesia Rukyaa aula CAF

0
477

Kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) imetaja majina ya waamuzi 29 wakiwemo watatu wa kike watakaochezesha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini mwezi Aprili mwaka huu.

Katika orodha hiyo wamo waamuzi wa Kike Watatu ambapo itakuwa mara ya kwanza, kwa waamuzi wa kike kuchezesha fainali hizo na watahudhuria mafunzo maalum yatakayoanza Machi 31 hadi Aprili 4 mwaka huu  nchini Morocco.

Waamuzi waliopata bahati hiyo ni Jonesia Rukyaa kutoka Tanzania ambaye ni mwamuzi pekee wa kike katika orodha ya waamuzi 15 wa katikati waliotangazwa.

Wengine ni waamuzi wasaidizi Mary Njoroge kutoka Kenya na Lidwine Rakotozafinoro kutoka Madagascar ambao ni waamuzi pekee wa kike kwenye orodha ya waamuzi wasaidizi 14 waliotangazwa.

Mataifa yatakayoshiriki fainali hizo zitakazoanza kutimua vumbi Aprili 14 hadi 28 mwaka huu jijini Dar es salaam ni wenyeji Tanzania, Nigeria, Angola na Uganda yaliyopangwa Kundi A, wakati Guinea, Morocco, Senegal na Cameroon  zikiwa kundi B.