Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekenolojia William Ole Nasha amesema kuwa serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imefanikiwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa siku Tano wa Waratibu wa miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi 46 ambazo ni Wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA).
Amesema kuwa IAEA inafadhili miradi mingi katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ile ya sekta ya afya, ambapo imewezesha kupatikana kwa vifaa kadhaa vya uchunguzi wa tiba na maradhi ya saratani ambavyo vimefungwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza na hospitali ya Ocean Road iliyopo jijini Dar es salaam.
Pamoja na vifaa vya uchunguzi katika hospitali hizo mbili, pia taasisi nyingine zimepata vifaa vya maabara vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 6.2 na kutoa mafunzo kwa wataalamu katika eneo la matumizi ya mionzi na Teknolojia ya Nyuklia, mpango uliogharimu Shilingi Bilioni 3.3.
Naibu Waziri huyo wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amelishukuru na kulipongeza Shirika hilo la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya nchi Wanachama hasa kwa utaratibu wake wa kuwa na mikutano inayowezesha kubadilishana uzoefu baina ya wanachama.
Amewataka washiriki wa mkutano huo wa Kimataifa wa waratibu wa miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi Wanachama wa IAEA kuhakikisha wanafanya majadiliano yenye tija kwa lengo la kusaidia nchi zao kwenye udhibiti na matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA ) Profesa Shaukat Abdulrazak amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya Nyukilia kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za Afya , Kilimo,Mifugo,Maji ,Viwanda na Ujenzi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Nguzu za Atomiki Tanzania , Profesa Lazaro Busagara amesema kuwa tume hiyo imeendelea kuzichukulia hatua taasisi zote zinazokiuka taratibu za matumizi salama ya Mionzi na Teknolojia ya Nyuklia nchini ikiwemo kutokuwa na leseni, kutokuwa na wafanyakazi wenye utaalamu wa matumizi ya mionzi na teknolojia ya Nyuklia pamoja na Mionzi.
Ametolea mfano wa hospitali ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 walizifungia 112 zilizoshindwa kufuata masharti hayo, ambapo hospitali 40 kati ya hizo zimekidhi vigezo na kufunguliwa huku zingine 72 zikiendelea kufungiwa kutumia vifaa vinavyotumia mionzi.