Ole Gunnar aonja joto ya jiwe

0
432

Ole Gunnar Solskjaer amekumbana na kipigo cha kwanza kwenye Ligi Kuu ya England tangu achaguliwe kuwa kocha wa muda wa Manchester United baada ya kutandikwa mabao Mawili kwa nunge na Arsenal ambao wanapanda hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kiungo wa kimataifa wa Uswiss, Granit Xhaka mapema katika dakika ya 13 aliachia kombora kali lililotinga moja kwa moja wavuni na kumuacha mlinda mlango wa United, –  David De Gea akiduaa tu kabla ya Pierre-Emerick Aubameyang  kupigilia msumari wa mwisho kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 69.

Ushindi huo unawafanya The Gunners kuvuna alama 12 katika mechi 10  walizokutana na vigogo wanaoshika nafasi Sita za juu kwa msimu huu na sasa wapo alama moja nyuma ya mahasimu wao kutoka London ya Kaskazini, -Tottenham Hotspur wanaoshika nafasi ya Tatu huku kila timu ikisaliwa na michezo Nane kuhitimisha msimu.

Manchester United wenyewe wamepoteza mchezo wa kwanza ugenini kwa mara ya kwanza tangu Disemba 16 mwaka 2018 huku wakishindwa kutikisa nyavu kwa mara ya kwanza katika michezo 22 waliyocheza ugenini katika mashindano yote tangu walipofanya hivyo mwezi Mei mwaka 2018 dhidi ya West Ham.

Katika hatua nyingine mabao Sita kati ya Saba aliyofunga Granit Xhaka kwenye ligi ya England amefunga akiwa nje ya eneo ya hatari huku David De Gea yeye akifanya makosa yaliyozalisha mabao mara mbili kwa msimu huu na yote ni dhidi ya Arsenal.

Katika matokeo ya michezo mingine iliyochezwa Jumapili Machi 10 mwaka huu, majogoo wa jiji Liverpool wanazidi kuwafukuza vinara Manchester City katika mbio za kuwania ubingwa baada ya kuibuka na ushindi wa mabao Manne kwa Mawili dhidi ya Burnley wakati Eden Hazard akiiokoa Chelsea na kipigo kwa kuifungia bao la kusawazisha katika dakika ya 90 kwenye mchezo wa sare ya bao Moja kwa Moja dhidi ya Wolverhampton Wenderes.