Magwiji wa soka wamlilia Pele

0
158

Wachezaji manguli wa soka wa zamani na wa sasa wameandika jumbe mbalimbali kumlilia gwiji wa soka ulimwenguni Edson Arantes do Nascimento (Pele) aliyefariki Dunia usiku wa Desemba 29, 2022.

Mshindi wa kombe la Dunia 2022 na nahodha wa Argentina Lionel Messi ameandika “Pumzika kwa Amani,” akiweka picha ambayo amepiga pamoja na Pele. Mshindi wa kombe la Dunia 2002, Ronaldo De Lima ameandika ujumbe mrefu na kumalizia “ Pumzika kwa amani gwiji wa soka wa wakati wote.”

Nahodha wa zamani wa England, David Beckham amechapisha picha akiwa na Pele na kuandika “It was HIS beautiful game ⚽ obrigado e adeus descansa em paz meu amigo” akimuaga gwiji huyo wa soka na kumalizia kwa lugha ya Kireno akimaanisha asante na kwaheri, pumzika kwa amani rafiki.

Nahodha wa Ureno na mshindi mara tano wa Ballon d’Or, Christiano Ronaldo ameandika kuwa Pele “alikuwa mtu aliyewashawishi wengi kuupenda mchezo wa soka, hawezi kusahaulika na atakumbukwa milele na wote tunaopenda soka” na kumalizia “Pumzika kwa amani.”

Zinedine Zidane yeye ameandika kwa kifupi “Eterno Rei Pelé” akimaanisha Milele Mfalme Pele, huku Nahodha wa Brazil  Neymar Jr akiandika maelezo marefu lakini akielezea kuwa kabla ya Pele mchezo wa soka ulikuwa kama michezo ya kawaida lakini aliubadilisha na kuufanya kuwa mpira wa miguu.

Mlinzi wa zamani wa kushoto wa Brazil, Roberto Carlos amechapisha picha akiwa na Pele ana kuandika ujumbe wa kumshukuru Mungu kwa kumlete Pele Duniani na yote aliyoyafanya.

Kylian Mbappe ameandika “The king of football has left us but his legacy will never be forgotten. RIP KING,” akimaanisha mfalme wa kandanda ametuacha, urathi wake hatuasahaulika, pumzika kwa amani Mfalme.

Vinicius Jr amemwelezea Pele kama, mfano, mwalimu, kiongozi na mpenda watu, mchezaji aliyeubadilisha mpira wa miguu. Amemaliza kwa kusema “Nakupenda sana Pele.”

Nyota wa Norway na Manchester City, Erling Haaland amesema kuwa kila unachoona kinafanywa hivi sasa katika soka basi ujue Pele ameishawahi kukifanya, Pumzika kwa amani Pele.