Mahakama Kuu nchini imesema kuwa wafungwa wa makosa ya kawaida ya jinai wana haki ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu.
Mahakama hiyo imetamka haki hiyo kwa wafungwa baada ya kubatilisha kifungu cha 11(1) (c) cha Sheria ya Taifa Uchaguzi kinachoweka zuio kwa wafungwa wanaotumikia adhabu ya kunyongwa na wanaotumikia adhabu ya kifungo cha kuanzia miezi Sita.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Elinaza Luvanda leo Desemba 22 inatokana na shauri la Kikatiba lililofunguliwa na raia wawili, Tito Magoti na John Tulla ambao walikosa haki ya kupigakura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kutokana na kuwa mahabusu.
Magoti na Tulla walifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masijala Kuu, mwaka huu 2022, dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Jeshi la Magereza.
Walikuwa walidai kuwa kifungu hicho kinakinzana na Katiba Ibara ya 5(1) ambayo inaeleza kuwa kila raia wa Tanzania kwenye umri wa miaka 18 anayo haki ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.
Ingawa wadaiwa wakati wa usikilizwaji wakipinga madai hayo, walidai kuwa NEC imekuwa ikiwawezesha raia wote kutekeleza haki hiyo kwa mujibu wa sheria, lakini Jaji Luvanda katika uamuzi wake amekubaliana na hoja za Wakili Seka kwa niaba ya wadia kuwa kifungu hicho kuweka zuio hilo kwa wafungwa wote wanaotumikia adhabu kuanzia miezi Sita kinakiuka Ibara ya 5(1) ya Katiba ya nchi.