Kikosi cha Stars kitakachopambana na Uganda chatajwa

0
657

Kocha wa timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars) Emmanuel Amunike ametaja kikosi cha wachezaji 25 kwa ajili ya kucheza mchezo wa mwisho wa kufuzu kwa michuano ya Afrika dhidi ya Uganda.

Katika kikosi hicho Amunike amemuacha mlinzi wa kati wa timu ya Baroka FC ya Afrika Kusini, -Abdi Banda ambaye inasemekana alitofautiana na kocha huyo kwenye mchezo uliopita dhidi ya Lesotho ambao Taifa Stars ilipoteza kwa bao moja kwa bila.

Kocha huyo amewaita wachezaji wapya wanne kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho ambao ni mlinda mlango Menacha Mnata na mlinzi wa pembani  Vicent Philipo wote wa Mbao FC ya Mwanza , mlinzi wa kati wa Singida United, -Kennedy Wilson na kipa toka Malindi ya Zanzibar, – Suleiman Salula.

Kikosi hicho cha kocha Amunike  kina wachezaji Kumi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na Nahodha Mbwana Samatta wa Genk ya Ubelgiji ambaye ni kinara wa ufungaji wa magoli kwenye ligi ya nchi hiyo kwa sasa na wachezaji wanne wanaocheza soka Kaskazini mwa Afrika kwenye nchi za Misri na Morocco ambao ni Simon Msuva,Himid Mao, Shiza Kichuya na Yahya Zayd.

Mchezo wa Stars dhidi ya Uganda utachezwa hapa nchini Machi 24 mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na ni mchezo muhimu kwa Taifa Stars kwa maana kama ikishinda itakuwa imefuzu kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika baada ya kupita miaka 39.