Emery ajipa matumaini kuhusu kikosi chake

0
799

Kocha wa timu ya Arsenal ya nchini Uingereza, – Unai Emery amesema kuwa ana imani kikosi chake kitapindua matokeo ya kichapo cha mabao matatu kwa moja ilichokipata kutoka kwa Rennes ya Ufaransa,  kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Europa katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa nyumbani wa timu ya Rennes uitwao Roazhon Park.

Arsenal iliyolazimika kucheza pungufu baada ya mlinzi Sokratis Papastathopolos kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye dakika ya 41, ilifunga bao mapema kwenye dakika ya Nne kupitia kwa Alex Iwobi kabla ya Nenjamin Bourigeaud hajaisawazishia Arsenal kwenye dakika ya 41.

Nacho Monreal wa Arsenal akajifunga kwenye dakika ya 65 na kuitanguliza mbele Rennes kabla ya Ismaila Sarr hajamfunga bao la tatu kwenye dakika ya 88 na kuwafanya Rennes waondoke kifua mbele kwenye mchezo wa kwanza.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Arsenal, -Unai Emery amesema mchezo huo ulibadilika baada ya kuwa pungufu, hivyo anatumaini watacheza vizuri kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo kwenye dimba la Emirates.

Kwenye matokeo ya michezo mingine, Chelsea imeirarua Dynamo Kyiv mabao Matatu kwa Nunge kwenye mchezo uliochezwa Stamford Bridge kupitia mabao ya Pedro Rodriguez, Willian na Callum Hudson-Odoi.

Nao Dinamo Zagreb wameifunga Benfica bao Moja kwa Bila, Eintacht Frankfurt imelazimishwa suluhu na Inter Milan, Sevilla nayo imelazimishwa sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili na Slavia Praha huku Zenit Saint Petersburg ikibugizwa mabao matatu kwa moja na Villarreal.

Napoli wamewakandamiza Salzburg mabao matatu kwa sifuri huku Valencia wakiibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja mbele ya FC Krasnodar.