Rais Samia atunukiwa tuzo kwa kuandaa filamu ya Royal Tour

0
143

Rais Samia Suluhu Hassan amepewa tuzo ya Kimataifa ijulikanayo kama International Iconic Awards iliyotolewa na Taasisi ya International Iconic Awards ya India kwa kutambua mchango wake katika kuasisi na kushiriki kwa umahiri mkubwa katika programu ya Tanzania: The Royal Tour ambayo imekuwa na matokeo chanya kwa jamii inayomzunguka.

Tuzo hiyo imekabidhiwa leo jijini Dodoma na uongozi wa Miss Jungle International na Bega kwa Bega na Mama (BBMF) kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ili aweze kuifikisha kwa Rais  Samia Suluhu Hassan.

Akipokea tuzo hizo, Waziri Balozi Dkt. Chana amesema Rais Samia ametoa mchango mkubwa katika kuinua sekta ya utalii nchini hasa baada ya athari kubwa ya janga la UVIKO 19 akiongeza kuwa Filamu ya Tanzania The Royal Tour imesaidia kutangaza vivutio vya Utalii na kuvutia watalii wengi nchini.

“Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa natoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutunukiwa tuzo hii ya kimataifa, natoa shukran za dhati kwa Taasisi ya International Iconic Awards ya India, nchi ambayo ni maarufu katika soko la kimataifa la filamu duniani kwa kutoa tuzo hiyo kwa Mhe. Rais ambapo kwetu ni chachu ya kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji wa Programu ya Tanzania: The Royal Tour.

Aidha, Dkt. Chana ametoa wito kwa wadau wa utalii waendelee kutekeleza kwa vitendo malengo ya Tanzania: The Royal Tour ili kuweza kufikia azma iliyokusudiwa katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini na kushukuru Miss Jungle International ambao walipokea tuzo husika na kuja kuikabidhi kwa Rais.