Rais asema mambo yanaenda vizuri

0
3059

Rais John Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa juhudi za kujenga Tanzania mpya zinakwenda vizuri kutokana na mafanikio makubwa yaliyoanza kupatikana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utatuzi wa kero za wananchi.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo Agosti 18 aliposalimiana na wananchiwa liokusanyika katika njiapanda ya Bugando jijini Mwanza na Mjini Sengerema akiwa njiani kuelekea Chato mkoani Geita kwa mapumziko.

Amesema kuwa utekelezaji wa ahadi za serikali unakwenda vizuri ambapo katika kipindi kifupi cha miaka miwili na miezi 8 kumekuwa na kasi kubwa ya ujenzi wa viwanda vilivyofikia 73,060, Kampuni ya Ndege Nchini (ATCL) imefufuliwa, miundombinu ya barabara na madaraja inajengwa, watoto wanapata elimu bila malipo na mengine mengi ambayo yamechangia kupanua uwigo wa ajira na kukuza uchumi.

Akiwa Sengerema Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi ambapo amepiga marufuku viongozi wa halmashauri kuwanyang’anya bidhaa zao wafanyabiashara wadogo na badala yake ameagiza viongozi wote nchini kujielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi ikiwemo ukosefu wa soko la mazao yao.

Ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa Sengerema kudai kuwa halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikiwanyang’anya matunda aina ya nanasi wakulima na wafanyabiashara wanaouza matunda yao mjini.

Rais amemuagiza mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella kufuatilia na kutatua kero hiyo.

Kabla ya kukutana na wananchi wa Mwanza,
Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) ya hospitali ya Bugando jijini Mwanza akiwemo dada yake Monica Magufuli.

Amewashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa juhudi kubwa wanazozifanya kuwatibu wagonjwa na amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa hospitali hiyo ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.