Wanaotegesha mazao watahadharishwa

0
61

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amewatahadharisha wananchi wanaotegesha kwa kupanda mazao kwenye maeneo yanayotakiwa kulipwa fidia na Mgodi wa North Mara.

Dkt. Kiruswa ametoa tahadhari hiyo alipotembelea maeneo ambayo wananchi wametegesha kwa kupanda mazao katika mgodi huo wa North Mara uliopo kwenye kijiji cha Komalela wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Ameuagiza uongozi wa mgodi wa North Mara kuwasilisha taarifa ya wananchi waliotegesha mazao pamoja na vielelezo vyote kuthibitisha kwamba watu hao wamepanda mazao hayo baada ya shughuli za uthamini kufanyika.

“Tukishawajua hao na vielelezo vipo taarifa hiyo itakwenda kwa vyombo husika kuhakikisha kwamba wananchi hao waliotegesha wanachukuliwa hatua za kisheria sababu wamevunja sheria ya kuja kuwekeza katika maeneo yaliofanyiwa tathmini.” amesema Dkt. Kiruswa

Pia amesisitiza kuwa uthamini wa mali zote kwa ajili ya kupisha maeneo hayo kwa ajili ya uchimbaji madini tayari umefanyika kwa mujibu wa sheria na kanuni.

“Wapo baadhi ya wananchi wameshalipwa fidia na wengine wameendelea kubaki kwa madai kwamba fidia waliyopewa haitoshi na wakati uthamini ulipofanyika walikubali na kusaini na wengine wakalipwa.” amesema Dkt. Kiruswa