Njia rahisi ya kumaliza akiba yako Desemba

0
171

Asilimia kubwa ya watu huanza mwaka mpya na mikakati mikubwa kifedha na wengine kuifanikisha na wengine kuiharibu kwa kuweka mikakati mingi ya kujiwekea akiba na kushindwa kuisimamia.

Yapo mambo yanayoweza kukufanya usione kabisa mafanikio ya akiba uliyojiwekea mwaka mzima. Na ukiyafanya haya utakuwa miongoni mwa wale wanaolia ‘Njaanuary’.

Kuelekeza akiba yako yote kwenye sherehe za Desemba.

Kukutana na ndugu na jamaa ni jambo jema, litakuwa baya kama hutajiwekea kiasi cha matumizi wakati wa kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwani unaweza kujikuta umemaliza hadi akiba ya kurudi kwenye majukumu ya kila siku.

Kununua vitu dakika za mwisho.

Hakikisha unaanza mapema kununua vitu vya matumizi ya Krismasi na Mwaka Mpya. Kwa kawaida, bidhaa hupanda bei kuelekea mwisho wa mwaka kutokana na uhitaji kuwa wa wingi pia. ni vyema ukajipanga na kuanza kununua vile vyenye kuweza kudumu muda mrefu mapema.

Hakikisha huondoki kijijini bila kununulia kila mtu bia mbili mbili.

Ukitaka kujimaliza kabisa, hii ndio njia rahisi zaidi. Hukujiwekea akiba kuanzia Januari 2022 hadi sasa ili ukanunulia majirani, ndugu na wapitanjia pombe kuanzia ufike kijijini hadi unaondoka. Timizi malengo yako kwanza, nunua vinywaji kwa kiasi.

Hakuna maisha baada ya Desemba ndivyo unavyowaza kwa wakati huu ila kabla hujamaliza kupanga namna ya kufuja pesa zote ulizojiwekea akiba, Januari kuna ada za shule, kuna kodi ya mwenye nyumba ambaye naye ameshatumia pesa zake zote Desemba, kuna pesa ya nauli na mafuta ya kwenda kazini kila siku kwa mwezi mzima.

Fanya uamuzi sahihi, pangilia vyema pesa zako kujiepusha na madeni, mikopo na msongo wa mawazo baada ya kuisha kwa sherehe za mwisho wa mwaka.