Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee amewataka watumishi wa serikali mkoani humo kujitathmini kama wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
Meja Jenerali Mzee ametoa kauli hiyo wakati akifunga kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kilichofanyika mjini Musoma, ambapo amesema shughuli nyingi hazitekelezwi ipasavyo hali inayosababisha ucheleweshaji wa maendeleo kwa wananchi.
Amesema kuna maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na vikao vya RCC, lakini utekelezaji hakuna kutokana na kutowajibika kwa watumishi hao.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mara amesema, watumishi hao wa serikali wanatakiwa kujitathmini kwani haiwezekani kila wanapokutana wanajadili mambo ambayo yamekwishajadiliwa na hayana utekelezaji wowote.
Amewataka kubadilika na kutambua wajibu wao ili waweze kuwaletea Wananchi maendeleo.