Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), limefungia vituo vya mtihani 24, vilivyothibitika kufanya udanganyifu katika mtihani wa kumaliza daraza la saba uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa NECTA Athumani Amasi amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuwa, vituo hivyo vitafungwa hadi hapo baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji wa mitihani kitaifa.
Amesema NECTA pia imefuta matokeo yote ya watahiniwa 2,194 ambao wamebainika kufanya udanganyifu katika mtihani huo wa kumaliza darasa la saba uliofanyika Oktoba 5 na 6 mwaka huu.
Watahiniwa wengine 179 matokeo yao yamezuiliwa, na hao ni wale ambao waliugua ama kupata matatizo na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au baadhi ya masomo.
Kwa mujibu wa NECTA, watahiniwa hao wamepewa fursa nyingine ya kurudia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2023.