Rais Samia Suluhu Hassan amesema ipo haja ya kuwepo na uhuru wa kitaaluma, kwani elimu na maarifa vinabadilika kwa kila zama na kwamba maendeleo hutokea pale penye uhuru wa kitaaluma.
Dkt. Samia ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam mara baada ya kutunukiwa Shahada ya Juu ya Udaktari wa Heshima wakati wa mahafali ya 52 duru ya tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa ni jukumu la taasisi za elimu nchini kuleta maendeleo na kuimarisha uchumi wa Taifa kwa kutoa elimu stahiki.
Dkt. Samia amevihakikishia ushirikiano vyuo vikuu nchini na kusema kuwa serikali itaendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya elimu na itahakikisha haitamuacha yeyote nyuma kama ilivyo mikakati ya kidunia katika sekta ya elimu.
Aidha, amewataka wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenda kulitumikia Taifa lao, kuwa raia wema na kuendeleza uhusiano mzuri na chuo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Kikwete amesema, chuo hicho kimeendelea kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa, huku wanawake wakiwa wengi zaidi ya wanaume.
Jumla ya wahitimu 1,592 wametunukiwa shahada mbalimbali katika mahafali hayo ya 52 duru ya tano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.