Taasisi ya Benjamin Mkapa inaendelea kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na virusi vya Ukimwi na Ukimwi kwa ngazi ya jamii na vituo vya afya nchini.
Akizunguza mkoani Lindi kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba Mosi mwaka huu Meneja mradi wa uboreshaji wa mifumo ya huduma za afya kutoka taasisi hiyo Hendry Samky amesema, taasisi hiyo imeajiri vijana 2,500 wanaotoa huduma za afya na elimu kuhusu virusi vya Ukimwi na Ukimwi katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema asilimia 53 ya vijana hao wamekuwa watumishi katika kanda mbalimbali za utoaji huduma na hivyo kusaidia jamii kupata elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo.
Samky amesema vijana hao kupitia ufadhili wa taasisi ya Benjamin Mkapa walijiunga na vyuo vya elimu ya kati na kusoma fani ya uuguzi, mafunzo ya uuguzi, maabara na utabibu.
Vijana hao wamekuwa wakifanya kazi ya upimaji wa virusi vya Ukimwi katika afua ambazo zinafanyika ngazi ya jamii na kwenye vituo vya afya kwa kutoa huduma na pia wamekuwa wakihakikisha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wanaendelea kutumia dawa katika misingi ambayo inakubalika kulingana na miongozo.