RC Mara alia na wabunge kutohudhuria vikao

0
44

Mkuu wa mkoa wa Mara Meja Jenerali Suleiman Mzee amewataka wajumbe wa kikao cha bodi ya barabara mkoani humo kuacha mazoea ya kutokuhudhuria vikao hivyo ambavyo viko kisheria.

Amewataja wabunge mkoani humo kuwa ndio wanaoongoza kwa kutohudhuria vikao hivyo na badala yake wamekuwa wakiwatuma wawakilishi ambao ni Makatibu, jambo ambalo amesema si sahihi.

Meja Jenerali Mzee amesema kwa mujibu wa sheria na utaratibu wa vikao hivyo, Makatibu wa Wabunge si wajumbe katika vikao hivyo, lakini ndio wamekuwa wakihudhuria kila mara.

Amesema Wabunge ndio wawakilishi wa Wananchi, kwa hiyo ni muhimu wahudhurie vikao hivyo vya bodi ya barabara ya mkoa ili kuwasilisha hoja za wananchi pamoja na kuwatetea.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara Akyoo Lengai amesema suala la kutohudhuria vikao kwa Wabunge wa mkoa huo ni la muda mrefu huku akishangazwa na tabia ya Wabunge hao kutuma wawakilishi kwenye vikao muhimu vya mkoa lakini hawatumi wawakilishi Bungeni.

Kikao cha Bodi ya barabara mkoani Mara kinaendelea huku kikihudhuriwa na Mbunge mmoja tu wa jimbo la Bunda Vijijini, Boniphace Getere.