Waacha masomo na kwenda kuchimba madini

0
61

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde ameahidi kushughulikia changamoto ya wanafunzi katika halmashauri ya Tarime Vijijini mkoani Mara kuacha masomo na kukimbilia kufanya shughuli za uchimbaji madini.

Naibu Waziri Silinde ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule mbalimbali ndani ya halmashauri hiyo ya Tarime Vijijini kufuatia ombi lililotolewa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Hata hivyo pamoja na Naibu Waziri Silinde kuahidi kushughulikia changamoto hiyo, amewataka wazazi katika halmashauri hiyo kuwa mstari wa mbele katika kushughulikia jambo hilo.

Akiwasilisha ombi hilo kwa Naibu Waziri Silinde, Waitara alisema suala la wanafunzi kuacha shule na kukimbilia kufanya shughuli za uchimbaji madini linasababisha upungufu wa Wanafunzi kwenye shule mbalimbali zilizopo katika halmashauri hiyo ya Tarime Vijijini.

Amesema watoto wengi wamekuwa wakijihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini, na hivyo kupuuza shule kutokana na pesa wanazipata.

Kwa mujibu wa Mbunge Waitara, kijiji cha Nyamongo ni moja kati ya vijiji vilivyoathirika na changamoto hiyo na kuiomba serikali kusaidia kukabiliana nayo ili kuwanusuru watoto hao na adui ujinga.