Waliokufa Kilombero waagwa

0
706

Miili ya Watumishi Tisa wa Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi (LTSP) waliokufa baada ya gari waliyokua wakisafiria kuacha njia na kutumbukia katika mto Kikwawila wilayani Kilombero mkoani Morogoro imeagwa hii leo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula ndiye aliyeongoza mamia ya waombolezaji wilayani Kilombero,  kuaga miili hiyo.

Akizungumza wakati wa kuaga miili hiyo, Naibu Waziri Mabula amesema kuwa familia, serikali na taifa kwa ujumla imepata pigo kutokana na kupoteza nguvu kazi iliyokua tegemeo kubwa.

Ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali hiyo,  ili kama kuna mambo ya kurekebishwa yarekebishwa ili matukio kama hayo yasitokee tena.

Shughuli ya kuaga miili ya Watumishi hao Tisa imefanyika katika uwanja wa Taifa uliopo mjini Ifakara na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa mkoa wa  Morogoro na wilaya zote za mkoa huo.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mkuu wa mkoa Morogoro, – Dkt Steven Kebwe amesema kuwa Watumshi hao wametoa mchango mkubwa katika kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero kupitia programu hiyo ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi, Programu iliyo chini ya wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Miili Tisa ya Watumishi wa LTSP iliyoagwa ni ya Rudaya Mwakalebela, Silvesta Mwakalebela, Gloria Mziray, Shebly Shebly, Salome Lukosi na Sheila Stambuli.

Wengine ni Maria Kunyanja, Hassan Kayuga na Msafiri  Gerald  kutoka shirika la Plan international.

Majeruhi wengine wa ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mtakatifu Francis iliyopo Ifakara.

Wakati ajali hiyo inatokea, gari hiyo aina ya Land Cruizer ilikua  na watu 13.