Watumishi wa mahakama kote nchini wametakiwa kutenda haki wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.
Pia wametakiwa kuepuka vitendo vya rushwa na mambo ambayo ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Wito huo umetolewa wilayani Busega mkoani Simiyu na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma, mara baada ya kuzindua majengo 18 ya mahakama za wilaya mbalimbali nchini, uzinduzi uliofanyika kwa niaba katika mahakama ya wilaya ya Busega.
Jaji Mkuu amesisitiza suala la haki na uwajibikaji kwa watumishi wa mahakama ambao wamejengewa na serikali majengo ya mahakama za wilaya, ili kukidhi vigezo na hadhi ya mhimili wa mahakama nchini.
Baada ya uzinduzi wa majengo hayo ya mahakama ya wilaya, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amepanda mti katika viwanja vya mahakama ya wilaya busega na kuwahimiza wananchi kuendelea kupanda miti ili kutunza mazingira.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Busega, Gabriel Zakaria amesema, ujenzi wa mahakama hiyo ya wilaya utawasaidia wananchi wa wilaya hiyo waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda Bariadi kupeleka mashauri yao, sasa kuyapeleka katika mahakama hiyo mpya.