Watuhumiwa wa mauaji Ngorongoro waachiwa huru

0
104

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) amewaachia huru wananchi 24 wa tarafa ya Loliondo mkoani Arusha waliokuwa wakikabiliwa na kesi mbili ikiwemo ya kupanga njama ya mauaji na kufanya mauaji ya askari polisi aliyekuwa akiweka alama za mipaka katika Pori Tengefu la Loliondo ambalo kwa sasa linajulikana kama Pololeti .

Hayo yameelezwa na Wakili wa upande wa mashtaka Upendo Shemkole, wakati shauri hilo lilipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa ajili ya kutajwa.

Shemkole amesema Mkurugenzi wa Mashtaka hana nia ya kuendelea kuwashtaki watuhumiwa hao na kuomba kuondoa shauri hilo mahakamani kwa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai.

Baada ya ombi hilo Hakimu wa Mahakama hiyo amesema mahakama imeridhia ombi hilo na kesi hiyo kuondolewa na washitakiwa wote 24 kuachiwa huru.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni njama ya mauaji ambapo wanadaiwa kupanga njama ya kuua maafisa wa serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10 mwaka huu eneo la Ololosokwan wilayani Ngorongoro walisababisha kifo cha askari polisi mwenye namba G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Miongoki mwa watuhumiwa hao ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ngorongoro, Nderango Laizer pamoja na madiwani 10 wa wilayani humo.