Waziri Mkuu : Lazima mjenge majengo bora

0
151

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kujenga nyumba na majengo bora, ili kuendana na kasi ya maendeleo duniani na kuvutia wawekezaji nchini.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo katika uzinduzi wa Sera ya ubia ya NHC, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo mkoani Dar es Salaam.

Amesema Shirika la Nyumba la Taifa lina mamlaka ya kuhakikisha majengo inalojenga nchini yanakuwa bora na yanakidhi mahitaji kwa watu watakaotumia majengo hayo.

“Lazima mjenge majengo bora, muwe na wivu kuiga kutoka mataifa mengine hasa katika ujenzi sio vibaya, angalieni namna ya mataifa mengine yanavyofanya kwenye ujenzi wa majengo na nyinyi mchukue ili kujenga majengo ambayo yatakuwa ya kisasa na yatakayokidhi huduma kwa wahitaji.” amesema WazIri Mkuu Majaliwa

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amelipongeza shirika hilo kwa kubuni njia ya ubia ambayo itasaidia kuwakaribidsha wawekezaji ambao watavutiwa kuwekeza na kutoishia njiani katika miradi yao.

Awali Waziri Mkuu ametoa vyeti vya shukrani kwa baadhi ya kampuni ikiwa ni kutambua mchango wao katika kuwekeza kwenye miradi ya nyumba (Public-Private Partnership).