Maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU) yamepungua nchini kutoka watu 110,000 mwaka 2016/2017 hadi kufikia watu elfu 54 mwaka 2020/2021.
Kwa mujibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), idadi ya vifo vinavyotokana na Ukimwi nayo imepungua kutoka vifo elfu 64 mwaka 2016/2017 hadi kufikia vifo elfu 29 mwaka 2020/2021.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko alipokuwa akizungumzia na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yanayofanyika Desemba Mosi kila mwaka.
Mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kitaifa yatafanyika mkoani Lindi.
Maadhimishio hayo yataanza tarehe 24 mwezi huu ambapo kutakuwa na shughuli mbalimbali hadi Desemba Mosi mwaka huu ambapo itakuwa ndio kilele cha siku hiyo.