Watakiwa kudai huduma bora za Mahakama

0
102

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma ametoa wito kwa wananchi kuwa mstari wa mbele kudai huduma bora za kimahakama.

Jaji Mkuu ameyasema hayo mkoani Kilimanjaro wakati wa hafla ya uzinduzi wa majengo ya mahakama za wilaya za Mwanga na Same, hafla iliyofanyika katika viwanja vya mahakama ya wilaya ya Mwanga.

Amewaelekeza wananchi kutumia namba ya simu 0752500400 kuwasilisha malalamiko au maoni yao Makao Makuu ili yafanyiwe kazi na wasisubiri ziara za viongozi ndipo wawasilishe malalamiko au maoni yao.

Kwa watendaji wa sekta ya mahakama nchini, Jaji Mkuu amewataka kuwa waadilifu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.

Amesema hategemei kuona kuna ucheleweshwaji wa haki, mrundikano wa mashauri, kuahirishwa mara kwa mara kwa kesi na uwepo kwa viashiria vya rushwa.

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesisitiza matumizi ya TEHAMA katika kutoa huduma za kimahakama na kutaka majengo yote ya mahakama yatumike kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi kama vile kufahamu mwenendo wa kesi pamoja na kufahamu sheria na taratibu za mahakama kwa njia ya TEHAMA.

Aidha, ametaka majengo hayo mapya ya mahakama za wilaya za Mwanga na Same yaliyozinduliwa hii leo yakatumike katika kuwanufaisha zaidi akina mama ambao ndio kundi kubwa ambalo mashauri yao yamekuwa yakianzia katika mahakama za wilaya, na hivyo kuowaondolea adha ya kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta haki.