Kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika hii leo Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kimeelekeza wataalamu wa ndani kushirikiana na wale wa kutoka nje kufanya uchunguzi wa ajali ya ndege ya Precision iliyotokea katika ziwa Victoria tarehe 6 nwezi huu.
Taarifa hiyo imetolewa jijini Dodoma na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari ambapo ameeleza masuala mbalimbali yaliyojadiliwa wakati wa kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri.
Aidha Msigwa ameeleza kuwa kikao hicho kimeelekeza vitengo vyote vinavyohusika na majanga nchini viimarishwe ili viweze kusaidia wakati wa majanga.
Wakati wa kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri, Serikali imewaomba wananchi kuwa watulivu wakati uchunguzi ukiendelea, ili kubaini chanzo cha ajali hiyo ya ndege iliyotokea Bukoba mkoani Kagera na kusababisha vifo vya watu 19, ambapo 24 waliokolewa.
Kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri pia kimepokea taarifa ya awali kuhusu ajali hiyo ya ndege ya Precision na hatua zilizochukuliwa baada ya kutokea kwa ajali hiyo.