Leo Novemba 14 ikiwa ni Siku ya Kisukari Duniani, imeelezwa kuwa kuwanywesha watoto wachanga maziwa ya ng’ombe badala ya maziwa ya mama ni moja ya sababu zinazowaweka katika hatari ya kupata ugonjwa wa Kisukari.
Daktari George Mkira kutoka Hospitalu ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ametoa tahadhari hiyo na kuwaasa wazazi kuhakikisha watoto wachanga wanatumia maziwa ya mama, na kuepuka kasumba na imani potofu zinazowafanya kutowanyonyesha watoto wao.
“Watoto siku hizi wanaanza kulishwa maziwa ya ng’ombe baada tu ya kuzaliwa, hii ni risk [hatari] kubwa ya wao kuja kupata Kisukari baadaye,” amesema Mkira wakati akitaja mambo yanayochangia mtu kupata ugonjwa wa Kisukari.
Amesema Kisukari ni ugonjwa ambao mwili unakuwa na sukari lakini unashindwa kuitumia ambako kunasababishwa na kukosekana kwa kichocheo ambacho ni homoni ya Insulin au homoni hiyo kutokufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, ametaja sababu nyingine zinazochangia ugonjwa huo kuwa ni ulaji (vyakula vya mafuta) na unywaji pombe usiofaa, tabia bwete (kutokufanya mazoezi), uzito uliopindukia, maambukizi ya baadhi ya virusi ambavyo hushambulia Insulin na sababu za kijenetia.
Ameeleza kuwa Serikali imeziwezesha hospitali nchini kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuhakikisha uwepo wa madaktari bingwa, dawa na vipeperushi vinavyotoa elimu kwa wananchi ambao tayari wana ugonjwa huo na ambao hawana ili kujikinga.