Msanii maarufu mwenye asili ya Colombia, Shakira Isabel Mebarak Ripoll anatarajiwa kutumbuiza kwenye ufunguzi wa mashindano ya Kombe la FIFA la Dunia yanayoanza tarehe 20 mwezi huu jijini Doha.
Wasanii wengine ni pamoja na bendi maarufu ya Hip hop Black Eyed Peas na kundi maarufu kutokea Korea Kusini, BTS.
Shakira ambaye hivi karibuni ametengana na mume wake mchezaji wa Hispania, Gerald Pique, ametajwa kuwa ni Malkia wa Kombe la Dunia kwa upande wa soka, na hii ni mara yake ya nne kutumbuiza.
Mara ya kwanza alitumbuiza katika Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani akiimba nyimbo zake maarufu za Hips Don’t Lie na Bamboo alizomshirikisha Wyclef Jean.
Mwaka 2010 alikuja na wimbo wa Waka Waka katika Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini na mwaka 2014 alitumbuiza kwenye sherehe za kufunga Kombe la Dunia nchini Brazil na wimbo wake wa La la la la la.
Hivi sasa Shakira anatamba kwa nyimbo zake kama Monotonia na Te felicito ambazo zimepokelewa kwa kishindo kwenye majukwaa mbalimbali ya kidigitali.
Fainali za kombe la FIFA la Dunia mwaka huu zitafanyika katika miji kadhaa nchini Qatar kuanzia tarehe 20 mwezi huu mpaka Desemba 18 mwaka huu.