Bunge laahirisha majadiliano muswada wa bima ya afya kwa wote

0
167
Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson akiongozi kikao cha bunge.

Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu bungeni leo umeahirishwa kutokana na kuwepo mashauriano yanayoendelea kati ya Bunge na Serikali juu ya mambo ambayo mihimili hiyo haijaafikiana.

Muswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza katika bunge lililopita, ulitarajiwa kujadiliwa na kupitishwa leo ili kukamilisha sehemu ya bunge ya kutunga sheria hiyo inayotarajiwa kuanza kutumika Julai 1, 2023.

Akitoa taarifa hiyo leo asubuhi, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa muswada huo utapelekwa mbele ya bunge pindi mashauriano hayo yatakapokuwa yamemalizika.

“Tunaendelea na mashauriano katika hoja kadhaa ambazo zimeibuliwa na waheshimiwa wabunge na wadau kadhaa ambao walijitokeza mbele ya kamati, na Serikali inaendelea kutazama namna bora ya kuwahudumia wananchi kwenye eneo hili la bima ya afya.” amesema Spika

Muswada huo unalenga kuboresha huduma za afya kwa kuwezesha wananchi wote kuwa na bima za afya zitakazowahakikishia upatikanaji wa matibabu wakati wowote.