Waathirika wa Precision Air kulipwa bilioni 396

0
223

Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt. Baghayo Saqware amesema waathirika wa ajali ya ndege ya Precision Air watalipwa fidia zao haraka iwezekanavyo.

Akizungumza jijini Dodoma katika semina ya wabunge kuhusu usalama barabarani, Dkt. Saqware amesema ndege hiyo ilikuwa na bima halali ambapo ilikata kutoka wakala wa ndani na nje ya nchi.

Amesema fidia itakayolipwa kwa Shirika la Ndege la Precision ni zaidi ya dola milioni 50 za Kimarekani (shilingi bilioni 116) na waathirika watalipwa zaidi ya dola za kimarekani milioni 170 (shilingi bilioni 396).

Akichangia mada katika semina hiyo Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage ameonesha kushangazwa na maelezo kuwa wananchi hao watalipwa baada ya uchunguzi, akihoji uchunguzi upi wakati wote wameona tukio limetokea na watu 19 wamefariki dunia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuharakisha ulipaji fidia kwa waathirika.

“Ajali ile imetokea, waathirika tunajua ni kiasi gani, waliofariki ni kiasi gani, kwa hiyo tunaomba TIRA nendeni mkasimamie bima iliyokatwa katika shirika lile iweze kulipa watu wale wote, kwa maana waliofariki na walionusurika.” amesisitiza Vita

Watu 19 walifariki dunia na wengine 24 waliokolewa baada ya ndege ya Precision Air kupata ajali katika Ziwa Victoria wakati ikitua katika uwanja wa ndege wa Bukoba Novemba 6, 2022.