Mbunge na Spika wambana Waziri Nape

0
141

Kilio cha wananchi kuhusu vifurushi vya mawasiliano ya simu kimefika bungeni jijini Dodoma, ambapo Mbunge wa Iramba Mashariki Francis Mtinga amehoji kwanini wananchi wanapangiwa muda wa matumizi ya vifurushi wanavyonunua, huku akitaka ukomo wa muda uondolewe.

Akichangia mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/2024, Mtinga amedai kuwa kampuni za mawasiliano ya simu zimekuwa zikiwaibia wananchi, hivyo kumtaka waziri wa sekta husika apeleke bungeni mabadiliko ya sheria.

“Hivi ni kwanini bundles [vifurushi] zina expire [zina muda wa mwisho]? Simu ni ya kwangu, nimenunua bundle kwa fedha yangu, halafu unanilazimisha nitumie kwa muda unaoutaka wewe, hii ni kwanini Mhe. Spika?”. amehoji mbunge huyo

Akizungumzia hoja hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema, tuhuma zilizotolewa na Mbunge huyo za kampuni za simu kuibia wananchi si sawa.

“Bundle ni huduma ya ziada ambayo ina masharti ya muda, ndio maana kuna bundle la wiki, la mwezi na kuendelea. Ukitaka lisiishe kwa muda uko utaratibu wa kutumia ‘main tariff’ ambayo ukiweka mpaka utakapoimaliza, hata kama ukikaa nayo kwa mwaka mzima.” amesema Waziri Nape

Ameongeza kuwa anachoona yeye tatizo lililopo ni uelewa, na shutuma za wizi zinapotolewa zitaharibu uwekezaji mkubwa na huduma ya mawasiliano.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amehoji utaratibu wa baadhi ya kampuni hizo za simu ambazo badala ya kutoka 1GB, zinatoa 800MB, akitaka kujua huo ni utaratibu wa kibiashara, au wizi?.

Waziri Nape amesema kilichotokea ni kuwa kampuni ilipandisha gharama za vifurushi lakini haikufanya mabadiliko kwenye mabango yao, hivyo mteja aliponunua kwa kiwango cha kwenye bango, akaona kuwa ameibiwa. Hata hivyo amesema mamlaka husika inaendelea kufuatilia na hatua stahiki zitachukuliwa.

Akihitimisha hoja yake Mbunge Mtinga ametaka utaratibu uwe kama wa kununua umeme, kwamba hata mwezi ukiisha umeme ulionunua kama haujaisha unaendelea kuwepo hadi mtumiaji atakapotumia wote.