Miaka 30 jela kwa kumdhalilisha mwenye ulemavu

0
133

Mahakama ya hakimu mkazi Musoma mkoani Mara, imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Juma Ligamba (40) mkazi wa kijiji cha Kibubwa wilayani Butiama, kwa kosa la udhalilishaji.

Ligamba amehukumiwa adhabu hiyo baada ya kuthibitika kumdhalilisha binti mwenye umri wa miaka 19 ambaye ana ulemavu wa akili na viungo.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi mwandamizi wa mahakama hiyo Stanley Mwakihaba ambaye amesema mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo na hivyo anastahili kutumikia kifungo hichò kwa mujibu wa sheria.

Mwakihaba amesema Ligamba ametiwa hatiani kupitia kifungu cha 130 (2) (c) na 131 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Imedaiwa mahakamani hapo kuwa Ligamba alitenda kosa hilo Septemba 20, 2022 majira ya jioni katika kijiji cha Kibubwa wilayani Butiama.

Siku ya tukio mshtakiwa ambaye ni jirani wa binti huyo alifika nyumbani kwao baada ya kubaini mama wa binti huyo hayupo na hivyo kuingia ndani alipokuwa amelalala binti huyo na kuanza kumdhalilisha.