TCAA: Uwanja wa Bukoba ni salama

0
113

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA ) , imesema uwanja wa ndege wa Bukoba mkoani Kagera ni salama na una uwezo wa kuhudumia ndege yenye uwezo wa tani hadi 29.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Hamza Johari amesema, madai ya baadhi ya watu kuwa ndege ya Precision iliyopata ajali tarehe 6 mwezi huu ilizidi uzito na hivyo kushindwa kutua kwenye uwanja huo hayana ukweli wowote.

“Uwanja wa ndege wa Bukoba una uwezo wa kuhudumia ndege yenye uzito hadi wa tani 29, ndege ya Precision ilikuwa na uzito wa tani 18, kwa hiyo mtu anaekuja na hoja kuwa ndege ilizidi uzito hapana sio kweli.” amesema Hamza

Ameongeza kuwa watu wanaozungumza mabaya kuhusu uwanja huo hawautendei haki, kwani una vipimo sahihi, umekaguliwa na umekidhi vigezo vya kuhudumu katika usafiri wa anga.

Kuhusu uchunguzi wa ajali hiyo ya ndege iliyotokea katika ziwa Victoria, Hamza amesema, mamlaka zinaendelea na uchunguzi na yeye hana mamlaka ya kuzungumza.