Mgunda abadili mbinu kuwakabili Singida Big Stars

0
129

Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo dhidi ya Singida Big Stars huku akiwakosa nyota mbalimbali kutokana na sababu kadhaa.

Miongoni mwa nyota hao ni kiungo chaguo namba moja la Mgunda, Clatous Chama ambaye amefungiwa kucheza mechi tatu kutokana na kosa la kushindwa kusalimiana na wachezaji wa timu pinzani.

Tukio hilo lilifanyika Oktoba 23 mwaka huu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga.

Mgunda amebainisha kuwa taarifa hiyo ameipata huku akiomba wenye mamlaka wanapotoa maamuzi kuwafikiria na walimu wa timu.

“Wachezaji wote wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars, unajua ni moja ya timu ngumu ambazo zinashiriki ligi lakini ambacho ninaweza kusema maandalizi yamekamilika..” amesema Kocha Mgunda na kuongeza kuwa

“Wapo wachezaji ambao tutawakosa ikiwa ni pamoja na Jimson Mwanuke, Israel Mwenda hawa bado hawajawa fiti lakini kwa upande wa Clatous Chama tumepata taarifa zake tunaheshimu maamuzi.”

Miongoni mwa wachezaji wa Simba ambao wapo kwenye kikosi hicho ni Mzamiru Yassin, Joash Onyango, Kenned Juma, Erasto Nyoni na Sadio Kanoute.