Serikali yasema haijaathirika kwa kujitoa OGP

0
161
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi bungeni jijini Dodoma.

Serikali imesema uamuzi wa kujitoa katika Mpango wa Uendeshaji Serikali kwa Uwazi (Open Government Partnership-OGP) haujaathiri uendeshaji wa Serikali kwa uwazi.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deo Ndejembi amesema uendeshaji haujaathirika kwa kuzingatia ukweli kwamba Serikali inao utaratibu wa ndani wa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi wakati wote kwa kuwa na vyombo na taasisi zilizokasimiwa majukumu ya kusimamia na kufuatilia Sera ya Uwazi na Uwajibikaji.

Amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma.

“Suala la kujiunga na OGP ni hiari kwa nchi mwanachama na vilevile inaweza kujitoa kwa hiari. Kwa msingi huo Serikali iliamua kujitoa kwa hiari,” amesema Ndejembi

Ameongeza kuwa kwa ngazi za kimataifa, Serikali imeendelea kuwa moja ya nchi zilizoridhia mfumo wa kukaguana wa nchi za kiafrika APRM (African Peer Review Mechanism) ambao ulianzishwa mwaka 2003 na Kamati ya Wakuu wa Nchi za Kiafrika.