Tanzania yaanza mchakato wa kuunda Satelaiti yake

0
185
Naibu Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Eng. Kundo Mathew akijibu maswali ya wabunge wakati wa kikao cha sita cha mkutano wa tisa wa Bunge la 12.

Serikali imesema inatambua umuhimu wa nchi kuwa na satelaiti na kwamba katika mwaka huu wa fedha imeanza kuandaa utaratibu wa awali utakaowezesha kuunda na kurusha satelaiti yake angani.

Aidha, imesema ili kuwezesha kufikia azma hiyo tayari imeunda andiko dhana na kuunda timu ya watalaamu watakaoshauri aina ya satelaiti itakayorushwa angani itakayoendana na mahitaji halisi ya nchi.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza programu ya kuunda na kurusha setelaiti angani.

“Ni matarajio kuwa timu hiyo itakamilisha kazi ya uchambuzi na kuwasilisha mapendekezo yake Serikalini kwa hatua za kimaamuzi ndani ya mwaka huu wa fedha,” amesema Kundo

Akizungumzia kwa upande wa Afrika, Kundo amesema kuwa hadi sasa Afrika ina jumla ya satelaiti 41, na kuanzia mwaka 2016 ni satelaiti 20 tu ambazo zimekuwa angani, na kati ya hizio 41 ni tisa tu ambazo zimetengenezwa na zina taswira ya Kiafarika.