Zoezi la ufungaji hereni za kielektroni kwa mifugo lasitishwa

0
269

Serikali imesitisha kwa miezi mitatu zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kuweka hereni za kielektroni kwenye mifugo (ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda) hadi Januari 31, 2023.

Taarifa hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema, hatua hiyo inalenga kutoa muda wa kufanya tathmini ya zoezi hilo kufuatia uwepo wa malalamiko ya wafugaji juu ya mambo mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za kuweka hereni hizo.

Amesema tathmini hiyo itatoa mwongozo wa namna bora zaidi ya kuendesha zoezi hilo ambalo linalenga kuwezesha ufuatiliaji wa mifugo kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kuirasimisha kwa mfugaji mwenyewe, kukabiliana na magonjwa na kudhibiti kuhama hama kusikozingatia sheria.

Malengo mengine ni kuimarisha kosafu ya mifugo, kuongeza thamani ya mifugo sokoni, kuwezesha upatikanaji wa bima na matumizi ya mikopo kwa wafugaji, kufuatilia mifugo iliyoibwa na kuwezesha sensa ya mifugo.

“Bei ya kuweka hereni kwa mnyama mmoja ni TZS 1,750 kwa ng’ombe na punda na TZS 1,000 kwa mbuzi na kondoo, gharama ambazo zimelalamikiwa kuwa ni kubwa na kwamba zoezi hilo linaendeshwa kibiashara badala ya kihuduma,” ameeleza Waziri Mkuu

Tangu kuanza kwa zoezi hilo mwaka 2021, idadi ya mifugo iliyotambuliwa na kusajiliwa ni 5,068,616 sawa na asilimia 11 ya kutambua mifugo 45,000,920.