Waziri Mkuu: Tumedhibiti moto Mlima Kilimanjaro

0
253
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa taarifa ya masuala mbalimbali ya Serikali bungeni jijini Dodoma katika kikao cha tatu cha mkutano wa tisa wa Bunge la 12.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa zoezi la kuzima moto uliozuka katika Mlima Kilimanjaro Oktoba 21 mwaka huu linaendelea vizuri na kwamba hadi leo Novemba 3, 2022 wamefanikiwa kudhibiti moto kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo korofi.

Ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akitolea ufafanuzi masuala mbalimbali ambapo amesema zoezi la uzimaji moto linaendelea vizuri licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali kama vile upepo mkali unaosambaza moto, miinuko na makorongo makubwa, mrundikano wa mboji inayohifadhi moto kwa muda mrefu na uwepo wa mimea ya asili inayoshika moto kwa urahisi.

“Tukio hili limesababisha hofu, hasara, kuteketea kwa kilomita za mraba 33 za uoto wa asili, uharibifu wa mandhari ya ukanda wa juu wa hifadhi na kuteketeza viumbe mbalimbali,” ameeleza Waziri Mkuu

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuokoa maeneo muhimu ya utalii wa kupanda mlima na hivyo shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida.

Ili kukabiliana na majanga ya moto yanayotokea kwenye hifadhi ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kuunda kitengo ndani ya KINAPA NA TANAPA kukabiliana na majanga ya moto yanayotokea ndani ya hifadhi.

Pia, ameziagiza kuwekeza katika teknolojia ya kisasa hususani katika tahadhari, utambuzi na uzimaji moto na kuimarisha shughuli za doria na uokoaji kwa kushirikisha jamii na wadau.