Mbunge wa Bunda, Boniphace Getere amesema anatamani kuteuliwa kuwa Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) baada ya kueleza kasoro zilizojitokeza kutokana na usimamizi wa fedha za umma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Bunda mkoani Mara.
“Wananchi wanapopelekewa fedha na mama inawauma sana kuliwa kwa sababu miradi yao haitaenda. Mhe. Spika, sasa hivi tunafanyaje bungeni? Hivi kweli tunamlilia nani kila siku hii Serikali? Hivi si nimuombe mama [Rais Samia Suluhu Hassan] aniteue hata waziri wa TAMISEMI kwa siku moja?” amehoji mbunge huyo.
Katika mchango wake kuhusu Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Getere ametoa mifano ya ubadhirifu halmashauri hiyo wamepewa bilioni 1 na Rais Samia kwa ajili ya kujenga halmashauri ya wilaya ambapo milioni 626.62 wamepewa wazabuni ambao hawajapeleka vifaa.
“Yaani wamepewa tu, nenda mkanunue nenda mkanunue, bila ukaguzi, bila nini. LAAC imeomba kwenda Bunda, Mheshimiwa Spika naomba uwaruhusu waende, watakuletea madudu,” amesema mbunge huyo huku akiongeza kuwa “Mama ametoa milioni 467 kwa sekondari mbili […] wamekwenda kwenye kiwanda cha Dragon wamenunua bati moja kwa shilingi 69,140.”
Amehoji kuwa hela za umma zitaliwa mpaka lini huku akisema kuwa wanaokula fedha hizo kila siku ni wale wale. Ameshauri kuwa idara, wizara au taasisi yoyote ambayo haijatekeleza maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hadi Machi 30, bajeti zao zisipitishwe.