Lula da Silva ashinda uchaguzi wa Brazil

0
802

Rais wa zamani wa Brazil Luis Inacio Lula da Silva, ameshinda duru ya pili ya uchaguzi baada ya kumuangusha mpinzani wake Jair Bolsonaro ambaye ndiye alikuwa akishikilia kiti cha urais.

Lula da Silva ambaye ni mwanasiasa wa mrengo wa kushoto, ameshinda kiti cha urais baada ya kupata asilimia 50.9 ya kura zote zilizopigwa dhidi ya asilimia 49.17 ya kura alizopata Bolsonaro.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi, Lula amesema ushindi huo si wake peke yake ama chama chake bali ni ushindi wa vuguvugu la demokrasia ya vyama vya siasa nchini Brazil.

Amesema jambo la kwanza alilopanga kulifanya nchini Brazil, ni kuzijenga upya siasa za nchi hiyo.

Inacio Lula da Silva aliwahi kuhudumu mihula miwili katika kiti cha urais nchini Brazil, kati ya mwaka 2003 na mwaka 2010.

Hakuweza kugombea uchaguzi wa Rais wa mwaka 2018 kutokana na kupigwa marufuku baada ya kupatikana na hatia ya kupokea hongo kutoka kwa kampuni ya ujenzi ya nchi hiyo, kama malipo ya kandarasi na kampuni ya mafuta ya Petrobras.

Lula alikaa gerezani kwa siku 580, kabla ya hukumu yake kubatilishwa na kurejea kwenye siasa.