Viwanda vya mbao kuendelea kutumia mashine za zamani

0
737

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, – Constantine Kanyasu ameuagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuwaruhusu Wadau wa misitu nchini na ambao wana viwanda vya mbao,  kuendelea kutumia mashine za zamani za kuchakata mbao huku wakijipanga kununua mashine za kisasa.

Naibu Waziri Kanyasu ametoa agizo hilo mkoani Kilimanjaro, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya mbao wa mikoa ya Kaskazini, – Ibrahimu Shoo.

Awali Shoo alimuomba Naibu Waziri Kanyasu  wapatiwe muda wa kutosha  kwa ajili ya kujipanga kununua mashine  za kisasa za kuchakata mbao,  baada ya kuzuiwa kutumia mashine za zamani kwa madai kuwa zimekuwa zikizalisha taka nyingi na hivyo kusababisha upotevu wa mbao.

Kufuatia ombi hilo la Shoo, Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii ameielekeza TFS iendelee kutoa  leseni na  mgao wa vitalu vya miti  kwa wamiliki wa viwanda wenye mashine za zamani,  ili kuwapatia fursa ya kujipanga kununua mashine zinazozalisha taka chache wakati wa uchakataji wa mbao.

Hata hivyo amewaeleza Wadau hao wa misitu nchini na ambao wana viwanda vya mbao kuwa uamuzi wa  kubadili teknolojia ya kutumia mashine mpya zitakazosaidia kupunguza  hasara  ya upotevu mbao bado upo palepale.