Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) , Felix Tshisekedi pamoja na ujumbe wa kila upande wamefanya mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam ambayo yamelenga kukuza ushirikiano baina ya mataifa hayo.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya mazungumzo yao, viongozi hao wametaja maeneo waliyokubaliana kushirikiana ambayo ni;
- Miundombinu (reli na barabara)
Tanzania, DRC na Burundi zina mpango wa kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Kigoma, kwenda Burundi hadi DRC ambayo itatochea biashara na mwingiliano wa watu kati ya nchi hizo.
Aidha, Tanzania na DRC zimekubaliana kujenga ushoroba wa kati (central corridor) ambayo itaunganisha nchi hizo mbili.
2. Sekta Binafsi
Ili kukuza biashara, Serikali za pande zote zimekubaliana kuunga mkono sekta binafsi zinazowekeza, hatua ambayo inachochea ukuaji wa biashara, kudumisha udugu na kuzalisha ajira.
3. Mawasiliano, Posta na Teknolojia
Makubaliano kati ya Tanzania na DRC yamesainiwa leo kati ya nchi hizo ambayo yatashuhudia Tanzania ikipeleka Mkongo wa Taifa nchini DRC na kuchochea ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
4. Usafiri (anga na maji)
Rais wa DRC amekubali ombi la Tanzania kupitia kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) kuongeza safari katika miji mingine nchini humo.
Aidha, Tanzania inaendelea na zoezi la ujenzi na ukarabati wa meli katika Ziwa Tanganyika, ikiwemo MV Liemba na MV Sangara ili kurahisisha usafiri wa watu.
5. Ushirikiano wa Kimataifa
DRC na Tanzania zimekubaliana kushirikiana katika masuala ya kimataifa kwenye mambo yenye maslahi kwa wananchi wa mataifa yote mawili.
6. Biashara na Uwekezaji
Tanzania na DR Congo zimekubaliania kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi ili kukuza biashara.
Aidha, mazingira ya uwekezaji yataboreshwa ili kuvutia uwekezaji kutoka mataifa mbalimbali, ambapo kwa kuanzia Tanzania inajenga bandari za Kibirizi, Kalema na Katoshi ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo.
Pia Tanzania inajenga meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 na kukarabati meli ya mafuta zitakazorahisisha usafirishaji wa shehena za mizigo kwenda DRC.
7. Ulinzi na Usalama
Akizungumza Ikulu Dar es Salaam, Rais wa DRC,
Felix Tshisekedi
amesema kuwa bila kuwepo kwa amani na utulivu, miradi na mipango yote ambayo mataifa hayo mawili imeweka haitofanikiwa.
8. Kilimo na chakula
Tayari Tanzania imefungua ghala la chakula nchini DRC ambalo inalitumia kuhifadhi na kuuza nafaka mbalimbali, ghala ambalo linatumiwa na serikali pamoja na sekta binafsi.
Pia, nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na ukataji wa miti na shughuli nyingine za kibinadamu.
Ili kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa, viongozi wote wamewaelekeza mawaziri wa pande zote kuendelea kukutana na kufanyia kazi makubaliano hayo.
Ziara ya Rais Tshisekedi nchini imekuja kufuatia mwaliko aliopewa na Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara ya kikazi nchini DRC mapema mwezi Agosti mwaka huu.