Jitihada za ziada zinahitajika kutangaza vivutio vya utalii nchini

0
255

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Isdor Mpango ameziagiza Wizara za Utalii Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wa utalii kuelekeza jitihada zaidi kwenye wazo la Rais Samia la kutangaza vivutio vya utalii vipya na vilivyosahaulika nchini.

Dkt. Philip Mpango ambaye ndio mgeni rasmi wa SWAHILI INTERNATIONAL TOURISM EXPO-S!TE 2022 ameyasema hayo katika ufunguzi wa maonesho hayo yaliyofanyika viwanja vya Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa kufanya hivyo jitihada zaidi zielekezwe pia kwenye kutangaza utalii wa ndani na kushawishi wananchi wa rika tofauti kutembelea vivutio vilivyopo nchini.

Ameongeza kusema kuwa ili kufikia lengo lililowekwa la kuingiza dola za kimarekani bilioni 6 kutoka kwenye Sekta ya utalii inabidi kuongeza jitihada zaidi ambapo wananchi wanahamasishwa kutoa huduma zinazohitajika katika soko la Utalii.

Kwa upande mwingine ameziagiza taasisi za kifedha kuendelea kuboresha huduma za malipo kwa kuhamasisha matumizi ya Credit Card kwenye kufanya malipo na kutoa huduma.

Aidha, Dkt. Mpango ameziagiza taasisi za kiserikali kutambua maoni ya wadau na mahitaji ya sekta ya utalii.